Hesabu zinavyoibeba CCM

Kuna haja ya kufanya utafiti mwingi kuona namna Lowassa anavyokubalika sasa baada ya kujiunga na Ukawa

By Kelvin Matandiko, Mwananchi

Uchaguzi wowote ni hesabu. Hata uchaguzi mkuu ujao wa rais, wabunge na madiwani ni suala la idadi ya kura za ushindi na kushindwa; kwamba unaungwa mkono na watu wangapi na unakataliwa na wangapi.

Katika kipindi hiki cha kukaribia kulifikia sanduku la kura, watabiri, wadadisi na wachambuzi wa masuala ya siasa wanapotoa mitazamo yao nani kuibuka mshindi kati ya mgombea urais wa CCM na wa Ukawa, wanajikita katika hesabu. Wapo wanaosema CCM itapata kura nyingi na wengine wanasema Ukawa utaibuka mshindi.

Wote wanatumia viashiria vya historia ya upinzani Afrika kuingia Ikulu, ushawishi wa mgombea, upepo wa kisiasa na nguvu ya makundi ya vyama vinavyounda ushirikiano. Je, ushirikiano wa vyama vya upinzani uliowezesha kwingineko kuingia ikulu utawasaidia Ukawa unaoundwa na Chadema, CUF, NLD na NCCR-Mageuzi? Je, hesabu zinaonyesha wana wingi wa watu kuliko CCM? Maswali haya mawili na mengineyo ni muhimu kuzingatiwa na wachambuzi badala ya kutoa majibu yanayoegemea mapenzi ya vyama.

Hali ya siasa

Hali ya kisiasa nchini imebadilika. Kwanza, kuna mwamko mkubwa kwa vijana wengi kujitokeza kushiriki siasa, hususan wanaohitaji mabadiliko. Pili, CCM imepungua mvuto kwa wananchi.

Mwamko wa vijana unaonekana wazi kwa majadiliano kupitia teknolojia ya mawasiliano kama vile mitandao ya kijamii, simu na huduma ya vyombo vya habari ambayo kwa asilimia kubwa iko maeneo ya mijini. Baadhi wanatumia mazingira hayo kuaminisha kuwa mwaka huu, Watanzania wataipeleka Ikulu Serikali ya Ukawa.

Hata hivyo, hesabu za kitafiti bado zinaipa CCM nafasi kubwa ya kurudi ikulu. Kuna viashiria vya wazi vya tafiti vinavyoonyesha kuwa CCM itaendelea kushikilia madaraka mwaka huu, ikiwa na uwezekano wa kupata kura zaidi ya asilimia 50.

Tafiti mbalimbali

Utafiti uliofanywa na Shirika la Twaweza na ule wa kampuni maarufu duniani inayojihusisha na tafiti za siasa ‘Greenberg Quinlan Rosner’, unaonyesha hesabu za Ukawa kuingia ikulu ni kupitia mtaji wa Edward Lowassa.

Utafiti huo umeonyesha kuwa Lowassa amebeba mtaji wa asilimia 18 ya kura ambazo zitaongezea ushindi wa Ukawa, ambao una asilimia 42 kwa nafasi yake.

Takwimu zilizokusanywa na Twaweza, Septemba 2014, zilionyesha kuwa asilimia 42 ya watu kwa kipindi hicho hawakuwa wameamua watamchagua nani kati ya wale waliotajwa kuwa huenda wangegombea urais. Swali la kujiuliza ni je, ni mgombea yupi amefanikiwa kuteka idadi hiyo ya Watanzania mpaka sasa?

Utafiti huo unabainisha kwamba, endapo Watanzania wangepiga kura mwaka huo, CCM ingepata asilimia 54 ya kura zote. Kwa tafsiri nyingine, Lowassa bado hakuwa na nguvu zaidi ya chama, licha ya ushawishi aliokuwa nao.

Kupitia tafiti hizi mbili, tunaona picha ya mgongano katika hesabu za kuelekea uchaguzi mkuu, hivyo bado hatuwezi kutilia maanani kwa asilimia 100 kwamba Lowassa atashinda. Hivyo, kuna umuhimu wa kufanya utafiti mwingine kupima ushawishi wa Lowassa tangu ahamie Ukawa kwa kuangalia kama wafuasi na kada waliomkubali wamemfuata au wamebaki CCM na kama bado watampigia kura.

Nafasi ya mgombea

Mbali na hoja ya kitafiti, nyingine ni nafasi ya mgombea na uwezekano wa kukubalika kwake. Ili kupata kura za ushindi, lazima mgombea atazame ushawishi wake kwa makundi ya kijamii.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Emmanuel  Mallya ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Sayansi ya Siasa aliwahi kueleza aina ya makundi ya  wapigakura waliopo nchini.

Alisema: Kundi la kwanza ni la wananchi wanaotaka mabadiliko (upinzani). La pili ni wale wanaoamini uongozi uliopo madarakani (CCM); kundi la tatu ni wale wasiokuwa na upande wowote kwa kufuata upepo wa kisiasa.

Wagombea wanatarajiwa kuwa wengi, lakini kipimo cha kukubalika kwa wagombea wawili, Dk John Maghufuli na Lowassa kinaonekana kuwa na utofauti mkubwa. Kwa ushahidi wa kimazingira, upepo wa kisiasa na tathmini za wachambuzi wa siasa zinaonyesha kuwa Lowassa ana nguvu na anakubalika, hususan maeneo ya mijini kuliko Magufuli.

Dk Magufuli anaweza kubebwa vyema na kambi itakayotumika kumtangaza na urahisi wa kujiuza kwa Watanzania akilinganishwa na kambi inayotakiwa kumtangaza Lowassa kwa wananchi.

Wengi wanaotarajiwa kutumika kumnadi Lowassa ni walewale waliotumika kumchafua alipokuwa CCM. Je, kwa muda uliopo watatumia lugha ipi ili kuwashawishi wananchi wa mrengo wa kati (wasio na vyama) wawaelewe?

Hesabu za kitakwimu

Pamoja na nafasi nzuri ya kujinadi kwa Dk Magufuli, bado hesabu za kitakwimu zinaonekana kumsaidia. Mwaka 2012, Serikali ilifanya sensa na kubaini makadirio ya Watanzania milioni 24, watakaokuwa na sifa za kupiga kura. Kwa sasa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza idadi ya waliojiandikisha wamefikia zaidi ya milioni 24.

Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana aliwahi kusema mpaka kufikia mwaka huu CCM ina mtaji wa wastani wa wajumbe wa nyumba kumi nchi nzima (mabalozi) 970,000. Kama kila mjumbe atakusanya wapigakura kumi, basi CCM itakuwa imevuna kura milioni 9.7.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu mwaka 2012, Watanzania milioni 31,623,919, sawa na asilimia 70.4 wanaishi vijijini huku wale waishio mijini ni 13,305,004, sawa na asilimia 29.6. Mbali na hilo, asilimia zaidi ya 50 ni wanawake.

Kwa kutumia takwimu hizo, uzoefu na historia vinaonyesha kuwa wakazi wengi wa vijijini na wanawake, bado wameendelea kuwa wapigakura wazuri kwa CCM. Mfano mzuri ni matokeo ya uchaguzi wa kura za maoni, ambayo yaliashiria CCM kuingia Ikulu tena baada ya kupata ushindi wa jumla mitaa na vijiji 9,406, huku vyama vingine vya upinzani vikigawana nafasi 3,211.

Kinachotia matumaini kwa CCM hadi sasa ni uwezo wa Kinana aliyezunguka nchi nzima katika kila kijiji na kufanya kazi ya upinzani. Huo ni mtaji kwa chama chake kinachohitaji kujikusanyia wapigakura kwa asilimia kubwa.

Ukawa kwa upande wao hawajafika maeneo ilikofika CCM. Je, kwa muda uliobakia kufikia Oktoba 25, Lowassa na Ukawa watazunguka vijiji vyote nchini na kuuteka mtaji huo wa wapigakura?

Mfumo wa uchaguzi

Mfumo wa uchaguzi unaipendelea CCM. NEC chombo muhimu cha kusimamia uchaguzi haiko huru. Msimamizi msaidizi wa uchaguzi ngazi ya wilaya ni Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya anayeripoti kwa Ofisi ya Tawala wa Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ambayo iko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Jambo hili limekuwa likipigiwa kelele na wadau wa vyama vya siasa, lakini halijapatiwa ufumbuzi. Mwenyekiti wa NEC, hana mamlaka ya kuwafukuza au kuwachukulia hatua wakurugenzi waliovurunda kusimamia.

Hata mwenyekiti wa NEC ni mteule wa Rais ambaye ni mwenyekiti wa CCM anayehitaji chama hicho kirejee madarakani.

Wahadhiri wasaidizi wa UDSM, Elijah Kondi na Mohammed Bakari kutoka Idara ya Sayansi ya Siasa wamefahamisha kwamba, ripoti mbalimbali ikiwamo ile ya Taasisi ya Uangalizi wa Uchaguzin (TEMCO), imekuwa ikibainisha CCM kubebwa zaidi na mfumo wa Serikali.

Udhaifu wa upinzani

Nguvu ya Ukawa ilikuwa imeshaanza kuimarika zaidi baada ya wimbi kubwa la makada wa CCM kujiunga na Chadema, lakini matumaini ya Watanzania wanaohitaji mabadiliko ni makubwa zaidi kwa kundi la Ukawa.

Hata hivyo, kuna mdudu ameshaanza kuutafuna Ukawa. Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibroad Slaa yuko kimya huku Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, mwasisi wa umoja huo, amejiengua jambo linalojenga hofu ya kutofanikiwa harakati za Ukawa.

Dosari hiyo ni kubwa na inaweza kuwa ni mtaji mkubwa kwa mgombea wa CCM, Dk Magufuli kuingia ikulu kutokana na kupungua umaarufu wa Ukawa. Baadhi ya wachambuzi wanadai CCM hutumia udhaifu kama huo kuvisambaratisha kila wanapojaribu kuungana.

Kutokana na mazingira, viashiria na mifano ya kitafiti ni wazi CCM bado inayo nafasi ya kurejea ikulu, ingawa lazima ijizatiti kufanya kazi kupitia kampeni zake.
Via Mwananchi

Advertisements

Leave a Reply

Please log in using one of these methods to post your comment:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s